Hatua zitakazokusaidia kubadili maisha yako

Binadamu wote tunayo nafasi ya kukosea na kufanya vizuri katika kipindi chote cha maisha. Pale tunapofanya vizuri tunajipongeza na kupongezwa na watu na pale tunapojikuta tumekosea pia tunayo fursa ya kutambua na kufanya mabadiliko.

Maisha ni kama safari ambayo wakati mwingine huwezi kujua kule unakoelekea nini kitatokea kwa hiyo ipo nafasi ya kuruhusu mabadiliko kutokea katika maisha ya mtu. Wakati mwingine watu huchelewa kufikia mafanikio na kujikuta wakijilaumu kwa nini wamekosea.

Karibu tena msomaji wetu wa mtandao huu wa maisha ni fursa. Leo tutajikita zaidi kwenye mada ambayo nimeipa kichwa “HATUA 4 KUFANYA MABADILIKO MAISHANI” Nashukuru kwa kuendelea kutuamini na kufuatilia kazi zetu,kwani bila wewe kazi yetu haina maana.

Haijawahi kuwepo,haitakuwepo na wala hatakuwepo binadamu ambaye katika maisha yake yote ataishi bila kukosea. Kwa hiyo kukosea ni sifa muhimu sana katika maisha ya binadamu hata kama kwa njia moja huoni umuhimu wa kuweka matarajio ya kukosea.

Kuondoa matarajio ya kukosea ukiwa kama binadamu katika maisha ni sawa kabisa na kujaribu kushindana na upepo kwani ni kitu ambacho hakiwezekanani kwa vyovyote kuweza kuuzuia upepo usivume.

Huwezi kufanya mabadiliko pasipokuwepo na eneo au kitu cha kubadilisha. Tunafanya mabadiliko pale tunapokuwa na kitu ambacho kwa namna moja hakiwezi kukidhi kusudi la kuwepo kwake kwa hiyo tunahitaji kufanya mabadiliko.

Wakati mwingine neno mabadiliko limeonekana kuwa neno zito sana kiasi cha watu kushindwa kulichukulia kwa umuhimu unaotakiwa na kujikuta wanaliogopa. Pengine tulilainishe kidogo kupunguza ukakasi walio nao wengi, kufanya mabadiliko ni kufanya maboresho.

Hakuna jambo baya katika maisha kama mtu kujua kuwa ana mapungufu katika eneo fulani la maisha lakini anakubali kuendelea kuishi na mapungufu ambayo yako ndani ya uwezo wake kubadilisha na kufanya maboresho muhimu katika maisha, na kuleta matokeo chanya zaidi.

Inaweza kuwa unataka kufanya mabadiliko katika eneo la elimu,mahusiano,katika uchumi wako,kuacha tabia ya kupanga na kuahirisha mambo,unataka kupunguza uzito,unataka kuachana na tabia ya kutegemea njia moja ya kipato,matumizi mabaya ya muda n.k

Kitu chochote unachoendelea kufanya kila siku lakini wewe mwenyewe unachukia matokeo yake unahitaji kufanya maboresho katika hilo eneo. Wakati mwingine inaweza kuonekana ugumu wa kubadilika kwa sababu kwa muda mrefu kwa kujua au bila kujua ulianza kujifunza polepole na kufanya mazoezi na mwisho wa siku ukajenga tabia na imani na sasa imegeuka kuwa sehemu ya maisha yako.

Ukweli ni kwamba hata katika upande wa mambo mazuri unayofanya kila siku ambayo yanasababisha wewe mwenyewe na jamii inayokuzunguka kusherehekea matokeo yake,ulianza kwa kujifunza pole pole haijalishi kuwa ulikuwa unajua au hukujua kama unajifunza.Ulifanya taratibu na kurudia na kurudia,na kurudia na mwisho wa siku ikajengeka sasa kuwa tabia na imani.

Kumbuka ikisha kuwa tabia sasa unabobea na kuwa mtaalam katika eneo hilo.Tunao watu wengi wataalam waliobobea katika maeneo yasiyo kuwa rasmi kama eneo la matumizi mabaya ya muda,mahusianao mabaya na watu n.k

Ingawa ipo tofauti kati ya mtu mzima, mtoto au kijana mdogo kubadilika. Kila mtu anayo nafasi ya kufanya mabadiliko katika eneo fulani na kuboresha maisha akiamua. Hapa kuna hatua 4 ambazo zinaweza kukusaidia kufanya maboresho katika maisha ukizifuata kwa uaminifu.

Tambua eneo unalotaka kufanya mabadiliko
Huwezi kufanya mabadiliko yoyote kama hujui eneo ambalo unataka kufanya mabadiliko hayo.Hivyo hatua ya kwanza ni kuwa na uhakika wa eneo ambalo unataka kufanya mabadiliko.Unao uhakika ungeweza kufanya vizuri zaidi unavyofanya kwa hiyo unahitaji kuboresha ili maisha yawe na ladha zaidi.

Ukisha kuwa na eneo unalotaka kufanyia mabadiliko ili kuboresha maisha yako tengeneza sababu ya kufanya mabadiliko.Bila kuwa na sababu ya kufanya mabadiliko inawezekana usiweze kufika mbali sana na kujikuta unaishia njiani tofauti na ulivyolenga.

Ili safari yako hiyo ya mabadiliko iwe nyepesi basi hakikisha nyuma ya sababu kunakuwa na matokeo au maumivu yaliyosababishwa na tabia ya kurudia rudia kufanya kitu ambacho matokeo yake yamekuwa ni uchungu na fedheha kwako na kwa watu wengine. Maumivu ndicho kitu ambacho kitakufanya ufanye azimio la kutokuendelea tena katika hali ya namna hiyo.

Hesabu gharama
Ukishajua eneo la kufanyia mabadiliko,sababu na maumivu nyuma ya sababu hiyo kitu kingine ambacho unapaswa kukijua na kukifanyia kazi ni kuhesababu gharama ya mabadiliko unayotaka kuyafanya.Hii ni muhimu sana pia kwani bila kuhesabu gharama utajikuta unashindwa kufika kule unakotaka kufika na kurudia tabia yako ya siku zote na hapa kubadilika linaweza kuwa jambo gumu.

Tabia ni hali ambayo unaishi nayo kama sehemu ya maisha yako ambayo unairudia mara kwa mara.Umezoeana na tabia na hiyo tabia imezoeana na wewe kuliko ninavyoweza kueleza hapa.Hakuna kitu kigumu kama kubadili tabia kama hujui cha kufanya na pia hakuna kitu chepesi kama kubadili tabia kama unajua njia sahihi za kupitia kubadili tabia fulani unayotaka kuondokana nayo.

Weka mpango wa namna ya kutoka ulipokwama
Ukisha hesabu gharama sasa weka lengo na mpango wa namna ya kufikia azma yako ya kuleta mabadiliko katika matumizi mabaya ya muda na sasa kuwa na matumizi mazuri ya muda.Mpango ni utaratibu utakaojiwekea mwenyewe ili kukuwezesha kufika kule unakotaka kufika.Ni kama unalima barabara katika ulimwengu wa kufikirika na hatua ya mpango sasa itakusaidia kudhihirisha kile unachokiona katika ulimwengu wa roho kuwa katika ulimwengu wa mwili na nyama.

Weka kwenye matendo na fanya maboresho ya mkakati mara kwa mara
Mambo yote yaliyotangulia hapo juu yatakuwa na maana tu kama utakuwa na uwezo wa kuyaweka katika vitendo ili sasa uweze kufikia azma yako.Bila kuweka kwenye matendo itabaki kuwa simulizi kama simulizi zingine tu bila matokeo kuonekana.Kubadilili tabia ni hatua inayohitaji kung’ang’ana sana ili kuvunja ukuta wa mazoea na kuingia katika mazoea na tabia mpya itakayokusaidia kufikia hatma unayoikusudia.

Kadri utakavyokwenda utajikuta mara kwa mara unahitaji kufanya maboresho ya mkakati ulioweka ili kusudi ufikie pale unapopataka.Kumbuka tabia unayotaka kubadilisha imejengeka kwa miaka mingi na kujikuta ina kuwa sehemu muhimu ya maisha yako,utahitaji muda pia kutoka huko.

Wataalaam wanasema inachukua kati ya miezi mitatu mpaka siku 360 kubadili tabia mmnaweza kutofautiana kutoka mtu mmoja na mwingine kutegemeana na mazingira na namna mtu atakavyojielekeza kufika anakotaka kufika.

Nataka nikutie moyo tu kwamba inawezekana ukiamua.Inawezekana kubadilisha kabisa namna unavyotumia muda na kuhamia kundi la watu wanaojua kutumia muda wao vizuri.Inawezekana kabisa kutoka katika kundi la watu wanaoishi bila mpango na kuingia kundi la watu wanaoishi kwa utaratibu.Maisha nifursa na hakuna jambo gumu kufanya ili mradi uwe na dhamira ya kufanya jambo hilo.

Usisahau kujishukuru pale utakapokuwa umefanikiwa kubadilisha tabia ya zamani na kuwa na tabia mpya ambayo sasa itaanza kukupa matokeo chanya. Jishukuru hata kama unaona matokeo ni madogo kwa sababu huu ni mlango wa mafanikio.

Naamini utakuwa umepata kitu kupitia makala hii fupi. Ukiwa na uhitaji wowote au ushauri katika eneo lolote la kuboresha maisha yako usisite kuwasiliana nasi kupitia njia za mawasiliano hapo chini. Aidha kwa kutuma ujumbe mfupi wa maneno, whatsapp kupiga simu au kututumia barua pepe nasi tutarudi kwako mapema iwezekanavyo.

Comments

Popular posts from this blog

Mambo muhimu ya kuzingatia kabla ya kuomba mkopo

Mbinu za kuongeza mauzo katika biashara

Zijue aina za biashara unazoweza kuzifanya pasipo na mtaji